Kwa Chegho Ziwa Linaloelea Milimani Hatarini Kutoweka

By EM123456 September 6, 2016 41 views 0 comments
Journal image 21958

KWA CHEGHO: 'ZIWA' LINALOELEA MILIMANI HATARINI KUTOWEKA

Wilayani mwanga mkoani Kilimanjaro zipo hazina za kipekee za kitalii ambazo hazijafahamika. Pengine kama zingetafitiwa na kuchapishwa kikamilifu zingewekwa kwenye kundi la maajabu ya urithi wa kidunia na kulindwa ili zisitoweke.

Mojawapo ni "˜Ziwa' la Kwa Chegho lililo juu ya safu za milima ya Pare ya Kaskazini, kwa wakazi wengi wa maeneo hayo wanaona jambo la kushangaza kukuta ziwa likielea juu ya mlima kwa vile mara nyingi mkusanyiko wa maji hupatikana sehemu za tambarare.

Ndiyo sifa inayolifanye eneo hilo kuonekana kuwa moja ya maajabu ya dunia.Ajabu hilo linapatika kwenye misitu ya Kindoroko katika kijiji cha Kisangara Juu kata ya Ngujini na eneo la Kamwala ambao pia ni msitu wa hifadhi ulioko Kijiji cha Vuchama Ndambwe wilayani Mwanga.

MAAJABU
Wakazi wa vijiji hivi wanasema kuwa na ziwa juu ya kilele cha milima ama miinuko ni jambo la kipekee. Hata wao hushangaa lakini kinachowasikitisha ni maarufu huo haufahamiki.

"Kuna ekari zaidi ya 15 za matete ama magugu maji ambayo yamestawi ndani ya ziwa juu ya mlima wa Kindoroko na kulifanya eneo kuwa na tambarare kubwa la kijani ambalo iwapo utalikanyaga utatitia na kuna taarifa za watu na wanyama kuzama." Anasema Godwin Mndeme maarufu kama Ikore.

Huyu ni mhifadhi wa msitu huo na mkazi wa Vuchama Ndambwe, anayeeleza kuwa kwa Kipare magugu haya huitwa ibura , majia au ngaghe. Kwa baadhi ya watu magugu hasa ngaghe hutumiwa kuezekea mabanda ya mifugo.

Kwa Chegho kuna nyumba ndani ya mahandaki ambayo huenda yalikuwa makazi ya family ya Chegho Mrutu, ambayo ni asili ya jina la ziwa hilo . Chegho alilima na kufuga zama hizo, karibu miaka 200 iliyopita, anadokeza Ikore.

Mzee Ikore mwenye miaka 85 anaelezea maajabu hayo kuwa yalitumiwa kwa makazi ndani ya mashimo na kwamba kuna mahandaki mapana ambayo pia yana kina kirefu na kwamba huenda yalitumiwa nyakati za vita, kujikinga na moto au kufukuza wanyama wakali.

Lakini pia , yalikuwa maghala ya kutunza vyakula vya watu na mifugo wakati wa njaa. Anasema Kwa Chegho kuna sifa nyingine ya kipekee kwani ni chanzo cha maji cha wilaya nzima ya Mwanga kwa hiyo kila unapoukuta mto ukitiririsha maji fahamu umenzia hapo.

"Ukiona mto maeneo kama Kisangara, Kilomeni, Kwakoa, Kiruru, Usangi , Kifaru na Nyumba ya Mungu chanzo chake ni hapa. Unapotembea kufuata njia au korongo la kila mto ni lazima litakufikisha hapa." Anasisitiza.

"Kama utatembelea kuufuatilia utafika hapa Kwa Chegho ndiyo maana haya ni maajabu kwa eneo hili."

Anashauri Wizara ya Maliasili na Utalii, kutatifi eneo hilo na ikibidi kusafisha mashimo haya kwani inawezekana kupata safu nyingine kama ilivyo kwa Mapango ya Amboni mkoani Tanga.

Mzee huyo aliyeishi kijiji hapo kwa zaidi ya miaka 80 anasema Kwa Chegho ni chanzo cha miti inayohifadhi maji kama mikuyu, mivuno, miangwi na mgugu kama "˜majia' au masale mbayo huzua ukame.

Pia ni chanzo cha miti dawa, matunda na wanyama wa aina mbalimbali kama kima, komba na ndege wa asili wanaoishi na kupatikana eneo hilo pekee.

DINDWI LA MAAJABU
Pamoja na kuwapo kwa ardhi oevu mlimani, kuna dimbwi la maajabu liitwalo Mboramboji. Husomwa "˜m-mboramboji' kwa Kipare. Hii ni sehemu ambayo inaaminika kuwa binti aliyekuwa amefikia umri wa kuolewa alizama wakati anachota maji.

Ikore anakadiria kuwa lilikuwa na ukubwa wa zaidi ya eka tatu na lilijaa vivutio vingi kama ndege, majani, wadudu na mazingira ya ajabu yaliyokuwa yanaleta hisia za wasiwasi na hata furaha . Watu walifurahia
utulivu wa ajabu, ubaridi na maji yaliyokuwa yametuama lakini yanasafiri mbali.

Dimbwi la ajabu linasadikiwa kuwa lilikuwa linapeleka maji hadi Butu na Mbureni maeneo ya Ugweno kwenye kilimo cha mpunga na mahindi. Maji katika ardhi hiyo oevu yamepungua kwa kiasi kikubwa.

Ikore anasema kazi binadamu hasa ukataji misiti kwa ajili ya ujenzi wa shule , makazi, kuni, mbao , kilimo na ufugaji bila kujali miradi ya uhifadhi vimechangia uharibifu huo.

Anasema kuwa licha ya kwamba hakuna uthibitisho kuna madai kuwa miti ya mikaratusi iliyopandwa eneo hilo inakausha maji na kuongeza jangwa.

MAONI KITAALAMU
Ili kufahamu ukweli kuhusu eneo hilola Kwa Chegho Nipashe iliwasiliana na Ofisa wa Maji Bonde la Mto Pangani, ambalo linahusika na usimamizi wa rasilimali za maji ya eneo hilo, Mtoi Kanyawanah, aliyethibitisha kuwa ni eneo oevu (wetland) lililopo milimani.

"Ni kweli sehemu hili ni chanzo cha maji ambayo yametumika kulisha mji wa Mwanga kwa miaka mingi. Kwa hiyo eneo kubwa la wilaya hii linategemea Kwachegho kwa maji ya kunywa hili ni dhahiri."

KUTOWEKA
Hata hivyo, anatoa taarifa za kusitikisha kuwa eneo oevu la Kwachego ambalo awali lilikuwa na maji mengi tena ya kutosha linatoweka.

"Chanzo hicho kilikuwa na uwezo wa kutoa mita za ujazo 2,000 kwa siku hivyo kutoa mchango mkubwa kwa ustawi wa mji wa Mwanga. Miaka ya karibuni chanzo kimepunguza uwezo hadi kufikia mita za ujazo 500 kwa siku," anasema Kanyawanah.

Anaongeza kuwa upungufu huo unaashiria kutoweka kwa chanzo hiki na kwamba sababu kubwa ni athari za binadamu kama kukata miti, kilimo na kuchoma mkaa bila kusahau mabadiliko ya tabia nchi.

"Kiasi chanzo cha Kwachegho kinavyokauka sasa mji wa Mwanga unategemea zaidi naji ya visima vya kuchimba baada ya uwezo wa eneo hili kuzalisha maji kupungua." Anaonya.

Kadhalika anaongeza kuwa inasemeka kwa kipindi hiki ikifikia nyakati za kiangazi maji hayafiki tena mjini Mwanga. Anapoulizwa iwapo ni kawaida kupata ardhi hiyo oevu kwenye vilele vya milima badala ya eneo tambarare anasema, ni matokeo ya michakato ya kijografia iliyohusisha kuwa na udongo unaohifadhi maji, magugu, mboji na miamba.

Anasema majani ya magugu hayo yametengeneza mizizi iliyopenya ardhini , kadhalika sehemu hiyo imekuwa na mboji nyingi iliyoruhusu majani kustawi hivyo kuzuia maji yanayoingia humo yasitoweke na kuishia bali yaendelea kutoka kwa kiwango kinachotakiwa na kuyalinda yasikauke.

UTALII
Kanyawanah anasema hakuna uhamasishaji uliofanyika kuhusu utalii katika eneo hilo licha ya kuwa na uwanda mkubwa wa magugu na ardhi oevu hakujafanyika uhamasishaji wa miradi ya kitalii.

UTAFITI
Mkuu wa Idara ya Utafiti wa Chuo cha Rasilimali za Maji cha Rwegalula kilichoko Dar es Salaam, Livingstone Swilla, anapoulizwa iwapo watafiti wana taarifa kuhusu eneo hilo lenye sifa za kipekee miongoni mwa wakazi wa Wilaya ya Mwanga, anasema habari zake hazifahamiki na halijafanyiwa utafiti. Anaeleza kuwa hata hivyo, kama mtafiti wa mkuu wa idara hana taarifa za kuwapo kwa eneo hilo na kusema kuwa pengine wakati umefika wa kulitafiti na kufahamu jiogarafia yake.

Tafiti zitalenga kuangalia ubora wa maji, kitu kinachoyashikilia kwa muda mrefu na pia chanzo cha kupungua kwake nyakati hizi.

Related Surnames:
MRUTU

No comments yet.